Riziki Toleo la 1/2024 'linapatikana'
Cathbert Msemo
Yesu Kristo ni uhai wetu
Kulikuwa na babu mmoja ambaye alijulikana kwa hekima, busara na maarifa mengi. Wengi walimjia ili kupata maneno ya hekima, ushauri na hata upatanisho. Mjukuu wake mmoja aliamua kumjaribu ili aone kweli ana hekima, maarifa, ujuzi na busara kama wanavyomwona wengi. Hivyo alichukua kipepeo kiganjani mwake akisema, ”Nitakwenda kwa babu na huyu kipepeo, kisha nitafunga kiganja changu. Nitamwuliza babu, ‘Kipepeo huyu yuko hai au amekufa?’ Akisema yuko hai, nitamminya na kidole changu na kumwua, kisha nitamwambia, ‘Babu umekosa’. Akisema kipepeo amekufa, nitamwachia na kumwambia babu, ‘Umekosa, kipepeo yuko hai’.” Mjukuu alipoenda kwa babu yake na kumwuliza kama kipepeo yuko hai au amekufa, babu alimtazama usoni kwa tabasamu na kumwambia, ”Mjukuu wangu, maisha ya kipepeo huyu yako mikononi mwako! Ukitaka aishi ataishi, na ukitaka afe atakufa.”
Mada kuu katika toleo hili la kwanza la Riziki 2024 ni Yesu Uhai Wetu. Kama vile uhai wa kipepeo ulivyokuwa mikononi mwa mjukuu, ndivyo tunavyokumbushana kuwa uhai wetu uko mikononi mwa Yesu. Aliye na Yesu anao uzima; ambaye hana Yesu, hana huo uzima. Makala nyingine inahusu watu ambao walipewa sharti la kumtazama nyoka wa shaba ili wapone. Ujumbe wake ni huohuo: Waliotii walipona, na waliopuuza walikufa. Siku zetu duniani ni kama kivuli, wala taraji ya kukaa hapana (1 Nya 29:15). Lakini tumshukuru Mungu kwa-mba wote waliozaliwa mara ya pili wamepata tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo (1 Pet 1:3).