RIZIKI toleo la 4/2024 'linapatikana'
Cathbert Msemo
Unavukaje kwenye bonde?
Je, umewahi kupita katika nyakati ngumu kiasi cha kuona uko kwenye bonde la uvuli wa mauti? Wakati kama huo ulijisikiaje? Na ulikuwa unaona nini mbele yako? Katika maisha haya kupita au kupitishwa katika bonde la uvuli wa mauti si jambo la ajabu. Lakini swali ni je, unavukaje katika hilo bonde?
Rais Mstaafu Nelson Mandela amewahi kusema, “Hakuna njia rahisi mahali popote ya kupata uhuru, na wengi wetu inabidi tupite katika bonde la uvuli wa mauti tena na tena kabla ya kufika katika kilele cha kile tunachokiamini na kukitamani”.
Mada kuu katika toleo hili la nne la Riziki 2024 inasema, Katika bonde bado Mungu yupo? Ni swali ambalo ni muhimu kutafakari ili tuwatie moyo wale ambao wanapita katika hali ngumu na kukata tamaa. Ni msaada kwa wale ambao wanapita na watakaopita katika bonde la uvuli wa mauti na kuogopa kuwa hakuna tumaini tena kwa maisha ya mbele.
Ndani ya gazeti hili utakutana na kijana mmoja ambaye Mungu alimpaka mafuta kuwa mtawala angali mdogo. Tokeo lake lilikuwa maisha yake kuwa hatarini, kwa sababu mtawala wa wakati ule alimwona kijana huyu kama adui.
Zipo pia makala mbalimbali na ushuhuda wa kukutia moyo kusonga mbele katika wito ulioitiwa, bila kujali hali unazopitia. Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Ulimwenguni mnayo dhiki, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu” (Yn 16:33b).
Karibu kusoma RIZIKI ONLINE HAPA