RIZIKI TOLEO LA 3/2024 'linapatikana'
Cathbert Msemo
Mungu wetu anatupenda bila kujali tumeangukia mbali kiasi gani, na bila kujali tunawaza au kufanya mabaya kwa kiwango gani. Kama tunayo pumzi bado Mungu anaona uwezekano wa kuturudisha kwake. Yeremia anasema, “Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele: ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu” (Yer 31:3). Upendo wa Mungu ni mkuu kama unavyoshuhudiwa katika hamu yake na dhamira ya kwamba sisi tuishi naye milele.
Zaidi sana upendo wa Mungu umeshuhudiwa kwetu kwa njia ya tunu ya thamani ya Mwanawe pekee Yesu Kristo, ambaye alimtuma ili awaokoe wanadamu wote.
Mada kuu katika toleo hili la tatu la Riziki 2024 ni Mungu wa Agano. Tunakumbushana kuwa upendo wa Mungu kwa mwanadamu ni upendo wa kipekee ambao hauwezi kulinganishwa na upendo wa aina yoyote ile. Ahadi ya kwamba hatatuacha yafungamana na agano lake nasi. Kama tukitoka kwenye agano hilo, tumepoteza ahadi hiyo. Kwa njia ya agano, Mungu ametuweka kwenye mikono yake, na anatuangalia na kutulinda kila wakati tusipatwe na hatari yoyote.
Katika toleo hili utasoma habari za mtu mmoja ambaye Mungu alimwokoa yeye na jamaa yake. Kupitia mtu huyu, Mungu aliweka agano kwa ulimwengu akiahidi kuwa hataangamiza dunia tena kwa maji. Pia kuna makala na shuhuda nzuri za kujenga na kukukumbusha kuwa Mungu anakupenda, haijalishi hali yako ya sasa. Yeye katika neno lake anasema, ”Naam, hawa [akina mama] waweza kusahau [watoto wao wanyonyao], lakini mimi sitakusahau wewe” (Isa 49:15).
Karibu kusoma RIZIKI ONLINE bure kwa kubonyeza HAPA