Twende 1/2023 - Linapatikana
Cathbert Msemo
YESU ANASIKIA MAOMBI YETU
MPENDWA MSOMAJI
Ukiwa na hitaji fulani nyumbani, nadhani unamwomba mzazi au mlezi wako naye anakupatia. Kwa mfano, unaweza kusikia njaa ukamwomba mama chakula na akakupa. Au ukipenda nguo nzuri unamwambia baba, Naomba uninunulie hii nguo, akakununulia. Vilevile ukiwa shuleni, unaweza kumwomba rafiki yako penseli na akakupa ili uchore picha nzuri kwenye karatasi yako. Ukiomba kitu kwa mtu yeyote kwa unyenyekevu, huwa unapewa.
Mungu mwenyewe anatumia mfano huo anapotukaribisha tumletee maombi yetu. Katika Biblia imeandikwa, “Ombeni, nanyi mtapewa”. Tukimwomba, ndiye Baba mwema anayetupa. Yeye ni zaidi ya wanadamu, maana anatupa zaidi ya yale tuombayo na zaidi ya tuwazavyo. Yeye anajua haja zetu hata kabla hatuja-mwomba, na hutupa kwa mapenzi yake mwenyewe.
Maombi yanamkaribisha Yesu ndani yetu. Yanatupa nafasi ya kuzungumza na Mungu kwa karibu zaidi – kama mtoto anavyoongea na baba mzazi anayempenda. Maombi yanajibiwa kwa mapenzi ya Mungu kwetu. Mungu anatupenda, na anatukaribisha tumwombe lolote tutakalo naye atatupa. Basi ukiwa na jambo lolote, nenda katika maombi umweleze Mungu naye atajibu.
Karibu usome toleo hili linalofafanua zaidi juu ya kujibiwa maombi. Linauzwa Tsh. 500 tu, katika Maduka ya Soma Biblia