RIZIKI TOLEO 1/2023 - Linapatikana
Cathbert Msemo
Kila mtu ana ushuhuda
Wakristo hatuna hadithi mmoja tu, bali tunazo hadithi nyingi za matendo makuu ya Mungu. Ushuhuda wetu ni hadithi za nguvu na uwezo wa Mungu katika maisha yetu. Kila siku mpya katika maisha yetu huleta hadithi mpya za wema na neema ya Mungu. Hivyo ni sawa kusema kwamba kila mkristo ana hadithi binafsi ya kusimulia, hasa tunapokumbuka kuwa Mungu ametuita mahususi, kama watu maalum na muhimu. Hadithi ya maisha yako ni ushuhuda wa wema wa Mungu, neema yake, na msamaha wake.
Katika toleo hili la Riziki tunajadili kichwa kisemacho, “Kuishi maisha ya ushuhuda’’. Lengo ni kukumbushana kuwa kila mmoja wetu anayo hadithi ya kushuhudia. Hadithi yako kuhusu kutembea na Kristo au changamoto ulizokutana nazo maishani zinaweza kufundisha, kujenga na kubadilisha maisha ya mtu mwingine anayepita kwenye hali kama yako.
Ndani ya toleo hili la Riziki utakutana na kijana mmoja ambaye hadithi yake haisemwi sana, lakini kidogo alichotuachia kina maana kubwa sana. Kijana huyu aligundua kuwa mchumba wake ni mjamzito. Sheria ya kwao ilikuwa wazi kuwa mwanamke aliyefanya jambo kama hilo alistahili adhabu kali. Lakini kijana huyu aliazimia tofauti. Unataka kujua kilichotokea? Fungua usome!
Pia utakutana na mada mbalimbali na shuhuda zitakazokusogeza mbele katika maisha yako ya kutembea na Kri-sto. Nami nasema, “Shuhuda zako, [Bwana], nimezifanya urithi wa milele; maana ndizo changamko la moyo wangu” (Zab 119:111).
Bonyeza hapa kusoma bure - RIZIKI ONLINE