Twende toleo 2/2024 'Linapatikana'
Cathbert Msemo
Yesu ni rafiki yangu
Hapa duniani ni vigumu sana kuishi peke yako. Daima utazungukwa na jamii inayojumuisha wazazi, walezi, ndugu na rafiki. Kila mmoja ana nafasi yake katika maisha yako.
Lakini wale tunaowaamini zaidi na kujikuta huru kushirikiana nao katika mambo yote, hata yaliyo ya siri, ndio huwachukulia kama rafiki zetu. Rafiki anaweza kuwa miongoni mwa ndugu yako au mtu wa mbali kabisa.
Sisi Wakristo tuna baraka kubwa sana. Tunaye mmoja aliyetuchagua sisi kuwa rafiki zake. Ni mwaminifu na yupo pamoja nasi kila wakati. Rafiki huyo ni Yesu. Yesu alitukomboa kwa kumwaga damu yake msalabani ili sisi tupate kuwa huru na utumwa wa dhambi. Huu ni upendo mkubwa sana sivyo?
Angalia Yohana 15:13-14 inavyosema, Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.
Karibu kusoma toleo hili ujifunze zaidi juu ya Yesu rafiki yetu. Makala zote zinafafanua vizuri jambo hili. Vijana mtajifunza pia namna ya kuchagua rafiki wa kweli kupitia makala ya Sala ya Vijana. Usisahau michezo na vibonzo vya kusisimua.