RIZIKI toleo 2/2024 'Linapatikana'
Cathbert Msemo
Hawakuwa watu maarufu
Kazi nyingi wanazopewa watu ni kutokana na ujuzi au mahitaji ya kazi yenyewe. Ndiyo maana kuwa na usaili ili mwenye kazi ahakikishe kuwa amepata mtu sahihi wa kufanya kazi yake. Kwa umuhimu wa kazi husika, matangazo yake yanatolewa hadi kwenye radio, runinga, magazeti na hata mitandao ya kijamii. Lengo ni kupata mtu sahihi kwa imani kwamba uzoefu wake, elimu yake na sifa nyinginezo zitaweza kuwa msaada kwa mahitaji ya mwenye hiyo kazi.
Swali tunaloweza kujiuliza ni kwa nini wakati Yesu ali-pochagua wanafunzi wake hakuchagua wasomi na watu wenye ujuzi wa mambo ya dini ili ujuzi wao umsaidie katika huduma yake hapa duniani? Na je, alitumia vigezo gani kuchagua wanafunzi ambao aliwaachia kuhubiri Injili baada ya yeye kurudi mbinguni?
Mada kuu katika toleo hili la pili la Riziki 2024 ni agizo la Yesu, “Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”. Lengo kuu la mada hii ni kukumbushana wajibu aliotuachia Bwana wetu Yesu Kristo wa kuihubiri Injili kwa watu wote. Anawatuma watu wote walioko tayari katika kufanya utume huu mkuu.
“Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako.” Huu ni mshangao wa walioitikia wito wa Bwana Yesu wa kuwafikia watu wote kwa Injili. Utapata kusoma pia habari za mmoja aliyeitika alipotumwa kwenda kuhubiri Injili katika nchi ya mbali, na jinsi ambavyo Mungu alikuwa pamoja naye.
Je, uko tayari kusema, “Niko hapa Bwana, nitume mimi”? Bonyeza HAPA kusoma