RIZIKI TOLEO LA #2/2022
Cathbert Msemo
Swali linalotuhusu sisi sote
Je, Mungu anaweza kumwacha mwanadamu? Au je, kati ya Mungu na mwanadamu nani anaanza kumwacha mwenzake? Maswali haya huwa yanaibua mijadala mizito yenye mitazamo tofauti tofauti. Wengine husema, “Ndiyo, Mungu anaweza kumwacha mwanadamu”, na kuthibitisha hili kwa kuonyesha jinsi Yesu alivyolia msalabani akisema, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Lakini je, ni kweli kwamba Mungu anaweza kumwacha mwanadamu aliyemwumba kwa mfano wake?
Katika toleo hili la Riziki tunajadili mada isemayo, Je, Mungu anaweza kumwacha mwanadamu? Msingi wa swali hili unatokana na hali ambazo tunakutana nazo kwenye maisha. Kuna wakati unapita mahali pagumu na kufikia hatua ya kufikiri kwamba Mungu amekuacha. Bila shaka, wakati wa shida na uhitaji mkuu ungetamani kuona mtu unayehusiana naye vyema akiwa karibu nawe kukutia moyo na kukusaidia. Vipi usipomwona, unajisikiaje?
Utakutana pia na habari za kijana mmoja ambaye watu wa familia yake walimfanyia mambo mabaya, lakini Mungu alikuwa pamoja naye, na hata akawa mkombozi wa ndugu zake katika nyakati ngumu za njaa.
Utapata pia makala za kukutia moyo na kukufundisha, na shuhuda ambazo zitakusogeza karibu na Mungu. Katika yote unayopitia Mungu anakuambia, “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha” (Kum 31:6).
Karibu kusoma zaidi BURE HAPA