RIZIKI TOLEO LA 4/2023 linatatikana 'Yesu kristo Ni njia ya uzima'
Cathbert Msemo
Kuna njia moja tu
Katika ulimwengu wa leo kuna njia nyingi za kutumaini. Hutokana na kuwepo kwa dini nyingi, na wingi wa mitazamo na mawazo yanayotofautiana juu ya furaha ya milele na Mbinguni. Na kila mtu huamini ya kuwa amesimama katika ukweli kuhusu tumaini la furaha ya kudumu.
Wengi wetu wanapenda kuishi katika dunia hii kwa muda mrefu iwezekanavyo. Tena wengine wanatamani wangeishi milele katika dunia hii.
Mada kuu katika toleo hili la nne la Riziki 2023 ni Yesu Kristo ni njia ya uzima. Kuna njia nyingi, lakini tunakumbushana kuwa kuna njia moja tu ya kumwingiza mtu katika furaha ya kweli ya milele. Kuna ukweli mmoja tu umfanyao mtu kuwa huru. Kuna namna moja tu ya maisha itakayomfikisha mtu katika uzima wa milele. Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, ndiye Njia hiyo moja.
Kwa nini tuamini hivyo? Kwa sababu Yesu ndiye Kweli. Alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Tena ndiye Uzima. Alifufuka kutoka kwa wafu. Yeye pia ndiye atakayewahukumu watu wote siku ya mwisho.
Katika toleo hili utakutana na habari ya mtu mmoja ambaye aliamua kupita njia ambayo kwa desturi za kwao hakutakiwa kupita. Uamuzi wake wa kufanya hivyo ulileta mabadiliko makubwa katika jamii ile. Utapata pia mafundisho na shuhuda za kukusogeza karibu na Mungu. Kumbuka Yesu alivyotuambia, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yn 14:6). Hivyo tumfuate yeye aliye njia.