Twende toleo no. 3, 2018 linapatikana sasa
Cathbert Msemo
Siku moja kulikuwa na mtoto anayesherehekea siku yake ya kuzaliwa. Aliandaliwa keki kubwa. Ilikuwa siku yake ya kwanza kupewa keki, hivyo alikuwa na hamu sana ya kuila, lakini akaambiwa asubiri. Alihuzunika moyoni: Jamani keki yangu nisubiri?. Wakaanza kuimba, halafu akaambiwa kata keki na chukua kipande kidogo mlishe Baba na Mama, kisha ndugu zako. Kwa sababu alitamani awe wa kwanza, hakuwa na furaha, lakini ni kwa sababu hakujua itakuwaje, saa yake ya kulishwa keki ikifika.
Basi saa ikafika, na wote waliokuwepo wakamlisha keki wakianza Baba na Mama. Wakaokota kipande na kumlisha, halafu wakamwambia, Hii yote iliyobaki ni ya kwako. Utakula taratibu, na ukipenda utaweza kuwapa rafiki zako. Akaanza kucheka na kushangilia.
Mtoto mwenzangu, mambo mengi yanahitaji uvumilivu ili kufikia mwisho mwema. Ni hivyo pia kwenye safari yetu ya imani. Biblia inatufundisha uvumilivu kupitia mifano ya watu mbalimbali.
Karibu usome toleo hili ujifunze maana ya uvumilivu na faida yake kwetu. Pia utasoma jinsi Twende ilivyoanza na salamu zetu bodi ya uhariri tukisherehekea miaka 10 ya gazeti letu.