Katika yeye tuna Ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi
Anne Gihlemoen
”Ukombozi”, maana yake ni kwamba wewe umefunguliwa kwa sababu gharama ya uhuru wako imelipwa. Kuna mambo mengi yanayokufunga au kukulazimisha. Matatizo na mashaka yanalundikana. Pengine unahali nzuri kwa namna mbalimbali. Hata hivyo kuna mengi yanayokuhangaisha na kukutia wasiwasi. Ni mambo ya binafsi, au ni mambo yanayohusiana na wapendwa wenzako, usharika au nchi yako. Nyuma ya hayo mengi, ndiyo dhambi pamoja na matokeo yake vinavyokukabili. Dhambi yabomoa maisha, na hatimaye yatoa mauti kama mshahara. Kwa hiyo jambo la msingi kabisa ni hili: Kuwa huru mbali na dhambi. Neno la Mungu latufundisha kwamba uhuru huo sio tokeo la wewe kuzidi nguvu na kushinda dhambi, bali ni tokeo la kusamehewa dhambi. Hilo lawezekana mahali pamoja tu; kwa Yesu. Kama uko kwa Yesu, imeandikwa kwamba umo ”katika yeye”. Maana yake umo ndani ya Yesu, umeunganishwa naye na yote aliyonayo. Akuingiza katika ukamilifu wote wa wokovu wake. Ukiwa ndani yake, Yesu anakuambia: ”Unao ukombozi. Umesamehewa dhambi zako zote. Nimekulipia uhuru wako”. Damu ya Yesu ndiyo gharama ile iliyolipwa ili uwe huru. Bado unasikia nguvu za dhambi. Unaona matokeo yake ndani yako na pande zote za kukuzunguka. Lakini roho yako inashangilia: ”Nimefunguliwa, niko huru, ni mwenye heri. Damu ya Yesu imefanya dhambi kuniacha huru. Nimegundua chemchemi ya uzima na baraka. Asante, Bwana Yesu, asante daima dawamu!.”