Kitabu Kipya 'Ukalifa au Mauti' Kinapatikana
Cathbert Msemo
Hadi leo wako Wakristo wanaoumia na kuuawa kwa sababu tu wanamkiri Yesu Kristo. Labda hapa Tanzania matukio ya ugaidi hayajawa mengi, lakini tayari wako Wakristo wanaoumia na kuteswa. Katika nchi nyingine, mateso ni makali zaidi. Hatujui mambo yatakavyoendelea. Hata sisi tunaweza siku moja kujikuta mbele ya kumkiri Kristo na kufa au kumkana na kupona uzima wa mwili wetu.
Ukalifa au Mauti ni kitabu kinachosimulia habari za kuteswa kwa Wakristo wa Nigeria. Kinatukumbusha kuwaombea ndugu zetu wanaoteswa na kuuawa kwa ajili ya kumkiri Yesu Kristo. Pia kinatujengea msukumo wa kumshukuru Mungu kwa sababu tunaweza kumfuata Bwana Yesu kwa uhuru, kutumia muda mzuri tulio nao sasa kwa ajili ya kumshuhudia Mwokozi wetu kwa Waislamu na kuwa tayari kujibu vema ikitokea siku ambayo utalazimishwa kuamua kumkiri Kristo na kufa au kumkana na kupona uhai wa mwili wako.
Maana halisi ya neno Ukalifa ni makamu au mfuasi wa Mtume Muhammad katika nafasi yake kama kiongozi wa Waislamu. Hili ni neno la Kihistoria kwa ajili ya kiongozi wa Ummah (jumuiya ya Uislam). Neno hili lilitumika pamoja na cheo cha Jemadari mkuu wa wenye Imani yaani Waislamu. Tafsiri iliyoko kwenye kitabu hiki (UKALIFA AU MAUTI) ina maana ‘UWE MFUASI WA MTUME AU UKATAE UFE’.
Kitabu kinapatikana katika maduka yote ya Soma Biblia; Dar es Salaam, Arusha, Mbeya, Iringa, Mwanza.
Bei: Tsh 4000 tu